Ndani ya Maisha ya Upadre: Siri Nzito Kuhusu Robo Tatu ya Mapadre

 Jimbo Katoliki Moshi ndio jimbo lenye Mapadre wengi na lililotoa Maaskofu wengi zaidi nchini. Kama ambavyo mkoa wa Mara kila nyumba ina “Soja” ndivyo ambavyo Jimbo Katoliki Moshi karibu kila nyumba ina Padre, Brother ama Sister.



Hii inatokana na mambo kadhaa. Mosi ni Historia ya Mapema ya Uinjilishaji. Wamisionari waliingia Kilimanjaro mapema sana na Moshi ikawa mojawapo ya majimbo ya kwanza kuanzishwa, na hivyo kujenga misingi ya malezi ya wito kwa vijana. Pili ni Utamaduni wa Wachagga kuheshimu na kukumbatia dini. Familia za Uchaggani zinajisikia fahari vijana wao kuingia seminari kutokana na malezi ya kitaaluma, imani na nidhamu.


Tatu ni Uwekezaji Mkubwa katika Elimu. Kilimanjaro ndio mkoa unaoongoza kwa kuwa na shule nyingi za sekondari nchini. Na siyo leo, ni tangu zamani. Elimu bora na malezi ya kiroho yamekuwa msingi wa kuzalisha mapadre wengi. Nne ni uwepo wa Mashirika mengi ya kimisionari kama vile ALCP/OSS, CSSp, OFM Cap, Jesuits n.k. Mashirika haya yamesaidia katika malezi ya vijana na kuhamasisha wito wa kipadre.


Kati ya Maaskofu 41 waliopo kwa sasa, Maaskofu 10 wanatoka Jimbo Katoliki Moshi. Hii ni sawa na robo ya Maaskofu wote. Na kati ya Maaskofu Wakuu 7 waliopo nchini, watatu wanatoka Jimbo Katoliki Moshi. Hebu tuwafahamu kwa kifupi:


1. Askofu Mkuu, Yuda Thadeus Ruwa’ichi, OFM Cap. Alizaliwa kijiji cha Mulo, Kilema, Jimbo Katoliki Moshi tarehe 20 Januari 1954. Alijiunga na Shirika la Ndugu Wadogo Wafransiskani Wakapuchini (OFM Cap) na kupata daraja takatifu la Upadre mwaka 1981. Ana Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Theolojia na Sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Urbaniana, Italia. Ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam.

Mha. Yuda Thadei Ruwa'ichi OFM Cap 


2. Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya, OFM Cap. Alizaliwa kijiji cha Shimbwe, Uru, Jimbo Katoliki Moshi tarehe 9 Mei 1957. Alijiunga na Shirika la Ndugu Wadogo Wafransiskani Wakapuchini (OFM Cap) na kupata daraja takatifu la Upadre mwaka 1989. Huyu ana PhD mbili. Ya kwanza ni Shahada ya Uzamivu katika Lugha na Fasihi ya Kigiriki na Kirumi, kutoka Chuo Kikuu cha London. Ya pili ni Shahada ya Uzamivu katika Theolojia ya Kiroho (Spiritual Theology) kutoka Chuo Kikuu cha St. Anthony, Italia. Ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.

Mha. Beatus Kinyaiya OFM Cap


3. Askofu Mkuu, Isaac Amani Massawe. Alizaliwa kijiji cha Mango, Kibosho, Jimbo Katoliki Moshi tarehe 10 Juni 1951. Baada ya majiundio yake ya kiroho na kikanisa, alipata daraja takatifu la Upadre mwaka 1975. Ana Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uongozi wa Taasisi (Organizational Leadership) kutoka Chuo Kikuu cha Walsh, Ohio, Marekani. Ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha.


4. Askofu Rogatus Kimaryo, CSSp. Alizaliwa kijiji cha Mkuu, Rombo, Jimbo Katoliki Moshi tarehe 30 Oktoba 1956. Alijiunga na Shirika la Wamisionari wa Roho Mtakatifu (CSSp) maarufu kama Holy Ghost Fathers na kupata daraja takatifu la Upadre mwaka 1987. Huyu naye ana PhD mbili. Ya kwanza ni Shahada ya Uzamivu ya Sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Gregorian, Roma mwaka 1997. Ya pili ni Shahada ya Uzamivu katika Dini (PhD in Comparative Religion) kutoka Chuo Kikuu cha Louvain, Ubelgiji mwaka 2005. Ni Askofu wa Jimbo Katoliki Same.

Mha. Rogatus Kimaryo CSSp


5. Askofu Augustine Shao, CSSp. Alizaliwa kijiji cha Mengwe, Rombo, Jimbo Katoliki Moshi tarehe 25 Septemba 1951. Alijiunga na Shirika la Wamisionari wa Roho Mtakatifu (CSSp) maarufu kama Holy Ghost Fathers na kupata daraja takatifu la Upadre mwaka 1983. Ana Shahada ya Uzamivu katika Utafiti wa Maendeleo (PhD in Development Research) kutoka Chuo Kikuu cha Bonn, Ujerumani. Ni Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar.

Mha. Agustine Shao CSSp


6. Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS. Alizaliwa Kibosho, Jimbo Katoliki Moshi tarehe 9 Desemba 1952. Alijiunga na Shirika la Maisha ya Kitume na Kazi za Roho Mtakatifu (Opus Spiritus Sancti) na kupata daraja takatifu la Upadre mwaka 1986. Ana Shahada ya Uzamivu katika Theolojia ya Maandiko (PhD in Scripture Theology) kutoka Chuo Kikuu cha Urbaniana, kilichopo Roma, Italia. Ni Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi.


7. Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS. Alizaliwa Mashati, Rombo, Jimbo Katoliki Moshi tarehe 9 Januari 1966. Alijiunga na Shirika la Maisha ya Kitume na Kazi za Roho Mtakatifu (Opus Spiritus Sancti) na kupata daraja takatifu la Upadre mwaka 1997. Ana Shahada ya Uzamivu katika Theolojia ya Mafundisho (PhD in Dogmatic Theology) kutoka Chuo Kikuu cha Urbaniana, kilichopo Roma, Italia. Ni Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma.


8. Askofu Beatus Urassa, ALCP/OSS. Alizaliwa kijiji cha Keni, Rombo, Jimbo Katoliki Moshi tarehe 2 Agosti 1965. Alijiunga na Shirika la Maisha ya Kitume na Kazi za Roho Mtakatifu (Opus Spiritus Sancti) na kupata daraja takatifu la Upadre mwaka 1997. Ana Shahada ya Uzamivu katika Theolojia ya Maisha ya Kiroho (PhD in Spiritual Theology) kutoka Chuo Kikuu cha Teresianum, kilichopo Roma, Italia. Ni Askofu wa Jimbo Katoliki Sumbawanga.


9. Askofu Prosper Baltazar Lyimo. Alizaliwa kijiji cha Kyou, Kilema, Jimbo Katoliki Moshi tarehe 20 Agosti 1964. Baada ya majiundio yake ya kiroho na kikanisa hatimaye alipata daraja takatifu la Upadre mwaka 1997. Ana Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha St. Paul, kilichopo Ottawa, Canada aliyoipata mwaka 2011. Alikuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Arusha tangu mwaka 2014, na sasa ni Askofu wa Jimbo jipya la Bariadi.


10. Askofu Henry Mchamungu. Alizaliwa katika kijiji cha Legho, Kilema, Jimbo Katoliki Moshi tarehe 8 Januari 1965. Baada ya majiundio yake ya kiroho na kikanisa hatimaye alipata daraja takatifu la Upadre mwaka 1994. Ana Shahada ya Uzamivu ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Katholische Privat-Universität kilichopo Linz, Austria aliyoipata mwaka 2011. Ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam.


Hii ni taswira ya namna Jimbo Katoliki Moshi limekuwa kitovu cha malezi ya Mapadre na Maaskofu wengi nchini Tanzania, kutokana na historia yake ya mapema, utamaduni wa imani wa Wachagga, uwekezaji katika elimu na seminari, pamoja na mchango wa mashirika ya kimisionari. Ecclesia una, sancta, catholica et apostolica 🙏🏽

Joseph

Karibu tuweze kujadili na kupakua habari mpya zilizojili Afrika, Tanzania na pia hata Kidunia kwa ujumla

Chapisha Maoni

I, (taja jina lako/indicate your name)

Mpya zaidi Nzee zaidi