Shetani ni Nani?
THOMAS S KAFUMU-IGUNGA-TABORA.
Hivi shetani ni nani? Biblia humwita “Mungu wa ulimwengu huu.” Lakini alitoka wapi? Je Mungu alimuumba kama alivyo? Je, yeye ni roho aliyeanguka? Haya hapa ni majibu kutoka katika Neno la Mungu!
Shetani amekuwa somo lenye shauku kubwa kwa maelfu ya miaka. Amedhaniwa kuwa kama jini, mzuka, na zimwi. Ama kama mtu mwenye sura nzuri ya “kishetani” aliyevalia suti nyekundu, mwenye pembe na uma ya nyasi. Shetani hata amesimuliwa kuwa kama kitu kisicho dhahiri “aliye muhtasari wa maovu yote.” Au kama chanzo cha kila kitu kibaya watendacho watu. Huenda wengi wanaufahamu usemi “shetani alinifanya nitende.” Ingawa fikira hizi ni za kawaida, zote SI SAHIHI! Hata zinapojumuishwa pamoja, kwa kiwango kikubwa zinamwakilisha isivyo roho huyu mkuu aliyeanguka!
Wengi wanaojiita Wakristo hutoa risala ndefu, kwa sauti kubwa juu ya “yule mwovu mbaya wa zamani.” Makundi mengi yenye misisimko huendesha mikutano kwenye mahema, kampeni, mikesha na harakati za kidini mahali ambapo watu huambiwa, “Tunakwenda kumwangusha chini yule mwovu usiku wa leo.” Idadi kubwa ya watu huondoka katika mikutano hii wakiwa wameshawishika kabisa kwamba wamefanya hili.
Hawako sahihi! Hawajafanikisha chochote zaidi ya hisia za kitambo za kujiridhisha wenyewe. Kwa bahati mbaya, shetani pia huondoka katika mikutano hii akijisikia hata kutosheka zaidi kutokana na kile alichokishuhudia—na kukisababisha!
Ni wachache wanaoujua UKWELI juu ya shetani ni nani na ni nini. Kijitabu hiki kitafutilia mbali fumbo, mkanganyiko, ujinga, kisasili (hadithi za kubuni), ushirikina na nadharia zisizosahihi zinazogubika ukweli juu ya utambulisho na asili yake.
Kuvutiwa na Shetani Kunakoongezeka
Mara chache sana mtu atazunguka huku na huku pasipo kusikia na kuona vidokezo juu ya shetani au mapepo. Tulia kwa muda na ufikiri juu ya mara ngapi hili hutokea.
Fungulia runinga. Nenda kwenye nyumba za sinema. Tembelea duka la vitabu. Ni mara ngapi somo la shetani, mapepo, malaika au ulimwengu wa roho huongelewa au kuandikwa kwa jumla? Mifululizo mizima ya vipindi vya runinga hutengwa mahsusi kwa ajili ya masomo haya, na vingine zaidi vikitokea kila wakati. Kwa miaka mingi sinema zimemlenga (zimemfokasi) shetani. Lakini sasa zinakuja mara nyingi zaidi—na ni za ajabu zaidi, zenye vioja, ngeni, za kutisha na kutia hofu kuliko hapo awali!
Fikiria shani ya “Harry Potter.” Baadhi ya waandishi karibu kabisa hawaandiki juu ya kitu kingine zaidi ya ulimwengu wa roho, mara nyingi wakichanganya ufahamu wa uongo wa unabii katika njama yao—na majeshi ya mashabiki hununua kila moja ya vitabu vyao.
Ushetani na uchawi vinatekelezwa kwa wazi zaidi kuliko hapo kabla!
Mamilioni hutumia kiasi kikubwa cha fedha kupiga simu za moja kwa moja kwa watabiri, wasoma viganja, wanajimu, watazama bao, wasihiri, wapiga ramri na kundi lingine la wenye kuwasiliana na mizimu, kutaka kujua nini kitawatokea siku za usoni.
Shetani huuza—na watu wananunua zaidi kuliko hapo kabla!
Mkanganyiko Usio wa Lazima
Mtume Paulo aliandika, “Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu” (1 Kor. 14:33). Wakati MKANGANYIKO mkubwa umegubika utambulisho wa shetani, huhitaji kukanganyikiwa!
Biblia ndiyo msingi wa maarifa yote. Mara kwa mara utatusikia tukisema, “Futa vumbi lililofunika Biblia yako! Ichunguze kwa makini na uone ukweli halisi ambao umekuwepo wakati wote katika kurasa zake. Usiamini chochote kwa sababu tu tumekisema, bali kiamini tu ikiwa umekiona kimethibitishwa ndani ya Biblia yako.”
Biblia inabeba majibu ya maswali yote makubwa ya maisha! UKWELI DHAHIRI wa maagizo yake haufundishwi katika makanisa ya ulimwengu huu. Tangu mapema kama “Shule ya Jumapili,” wengi wanafundishwa kuamini kile ambacho kila mmoja hudhania kimo ndani ya Neno la Mungu. Kile ambacho Biblia husema kuhusu asili ya mwovu Shetani kitakushangaza. Lazima tuiache Biblia imfunue jinsi alivyo.
Paulo pia aliandika, “JARIBUNI mambo yote; lishikeni lililo jema” (1 The. 5:21), na “MPATE KUJUA hakika mapenzi ya Mungu, yaliyo mema, yakumpendeza, na ukamilifu” (Rum. 12:2).
Tutayachunguza mafungu yanayofafanua asili ya shetani na kwamba yeye ni nani. Ili kufanya hivi, ni lazima tuachane na fikira za kibinadamu na tukubali tu kile kinachoweza kuthibitishwa ndani ya Biblia!
Shetani Alitoka Wapi?
Shetani yuko hai na halisi. Biblia inamuita “mungu wa ulimwengu huu” (2 Kor. 4:4). Ufunuo 12:9 husema kwamba “audanganyaye ulimwengu wote.” Kwa hakika hii hujumuisha ukweli juu ya utambulisho wake. Lakini je wakati wote amekuwa shetani? Wakati wote amekuwa yule mwovu, muuaji, mwongo, mkuu wa giza mharabu? Je aliumbwa jinsi hiyo?
Hakuwa hivyo!
Maswali haya yanahitaji ufafanuzi. Yale ambayo utayasoma yatakusaidia uione picha kamili. Biblia humwelezea shetani katika maandiko mengi. Kijitabu hiki kimsingi kinachunguza mafungu yanayofafanua asili ya shetani. (Kijitabu chetu kikubwa, Ulimwengu Matekani, hujadili maandiko mengi yanayoelezea jukumu, mkakati na hila zake. Soma kijitabu hiki cha rejea upate kuelewa kwa ujumla namna shetani anavyotenda kazi.)
Mwanzoni Mungu aliumba makerubi watatu: Lusifa au Nyota ya Alfajiri (aliyegeuka kuwa Shetani), Mikaeli na Gabrieli. Kila mmoja alitawala theluthi ya mamia ya mamilioni ya malaika (Ufu. 5:11). Nyota ya Alfajiri na theluthi yake walitawala ulimwengu uliokuwa kabla ya Adamu. Yeye, pamoja na malaika zake, waliasi serikali ya Mungu, na leo anawaongoza malaika hawa walioanguka, au mapepo, kama mungu wa dunia hii.
Mwanzo 1
Mwanzo 1:1 inasema, “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.” Andiko hili linaweka jukwaa kwa ajili ya somo letu.
Kitabu cha Ayubu kinaeleza vyema wakati ambapo Mungu aliiumba dunia, miaka mabilioni iliyopita. Mungu alimuuliza Ayubu mfululizo wa maswali: “Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama ukiwa na ufahamu. Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua? Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake?…Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha?” (38:4-5, 7).
‘Nyota” hizi walikuwa malaika (Ufu. 12:4), pia wameelezewa kama “wana wa Mungu.” (Bila shaka, nyota halisi haziimbi.) Angalia kwamba inasema “wote” “walipaza sauti” na “kuimba pamoja.” Palikuwa hapajawa na mapepo wabaya bado wakati wa uumbaji katika Mwanzo 1:1.
Andiko hili linaonyesha kwamba nchi iliumbwa katika hali ya ajabu na maridadi. Kulikuwa na furaha tele na uimbaji. Sasa soma Mwanzo 1:2.
Fungu hili limetafsiriwa isivyo na haliakisi maana ya Kiebrania asili. Biblia ya King James Version inasema, “Nayo nchi ilikuwa ukiwa tena utupu.” Maneno matatu muhimu ya Kiebrania yametafsiriwa isivyo hapa, hivyo kuzuia, na kwa hakika kuficha, maana halisi ya fungu isionekane.
Neno lililotafsiriwa “ilikuwa” ni hayah. Katika Mwanzo 2:7, neno hili limetafsiriwa kwa usahihi “a’kawa,” na katika Mwanzo 9:15, “hayata’kuwa.”
Maneno kwa ajili ya “ilikuwa ukiwa, tena utupu” ni tohu na bohu. Yakitafsiriwa kwa usahihi, yanamaanisha “vurumai, katika mkanganyiko, ukiwa na utupu.” Kwa ufupi, nchi iliyoumbwa kamilifu (fu. 1), “ikawa vurumai na iliyokanganyikiwa” (fu. 2). Tohu na bohu yametafsiriwa kiusahihi katika Yeremia 4:23. Isaya 34:11, miongoni mwa sehemu zingine, inatafsiri usemi huu kama “mkanganyiko na utupu.”
Angalia Isaya 45:18, inayobainisha namna ambavyo Mungu hakuiumba dunia: “Maana BWANA, aliyeziumba mbingu asema hivi, Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa [tohu kumaanisha vurumai au utupu], aliiumba ili ikaliwe na watu.” Ni wazi kwamba dunia ilikuja kuwa vurumai baada ya Mungu kuiumba—katikati ya matukio yaliyoelezewa katika Mwanzo 1:1 na 1:2. Fungu la mwisho linaelezea KU-umbwa upya kwa dunia miaka 6,000 iliyopita, na fungu la 1 linaelezea uumbaji wa kwanza wa ulimwengu mzima ambao, kulingana na wanasayansi, ulifanyika kadiri ya miaka bilioni 17 iliyopita.
Zaburi 104:30 inasema kwamba Mungu “aufanya upya uso wa nchi.” Zile siku saba za juma la uumbaji ni wakati ambapo Mungu aliikarabati upya dunia iliyoharibiwa, iliyoumizwa, iliyokuwa kwa wakati huo imefunikwa kabisa na maji (Mwa. 1:2). Tutakuja kuona kwamba hii ilisababishwa na shetani. Matendo 3:19-21 hufunua kwamba ni Kurudi kwa Kristo tu ndiko kutakakoleta “urejeshaji [kurejesha] wa vitu vyote.”
Sasa tunajua kile kilichotokea. Lakini kilitokea kwa namna gani? Ni kwa namna gani dunia ilibadilika kutoka kuwa maridadi na kamilifu wakati wa kuumbwa hadi kuwa vurumai, iliyokanganyikiwa, ukiwa na utupu? Kwa kuwa Mungu si Mungu wa machafuko (1 Kor. 14:33), tunajua kwamba Hakuiharibu dunia. Basi ni nani au ni nini kilisababisha hili?
Isaya 14
Biblia hufunua ukweli muhimu juu ya somo lolote ikiwa mtu atasoma maandiko yote yanayohusika nalo. Tukiwa na hili kichwani, hebu tusome juu ya Nyota ya Alfajiri baada ya kuwa Shetani.
Isaya 14:12-15 inaelezea hadithi isiyo kifani iliyo na viashiria kuhusu mahali ambapo Nyota ya Alfajiri alishawahi kuwa, alichofanya na kilichomtokea. Soma kwa makini, ukizingatia semi maalumu zilizotiliwa mkazo: “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu: Nitafanana na yeye Aliye juu. Lakini utashushwa mpaka kuzimu [“kaburini”—mafungu ya 9 na 11], Mpaka pande za mwisho za shimo.”
Yule aliyeitwa “Nyota ya alfajiri” isingewezekana kwamba alikuwa mtu. Mambo aliyoyafanya hayawezi kutendwa na mwanadamu awaye yote. Ni shetani pekee “huyaangusha mataifa” na kwamba alisema “angepanda mpaka mbinguni.” Kwa hakika hakuna mtu ambaye angeweza “kushushwa mpaka kuzimu” kwa jinsi ilivyoelezewa hapa. Mwisho, hakuna mtu aliye na kiti cha enzi ambacho kingeweza kuwekwa juu kuliko “nyota za mbinguni.”
MUNGU huishi katika upande wa kaskazini wa mbingu au “pande za kaskazini.” Ayubu anaangazia jaribio la Nyota ya alfajiri la kutaka kumpindua Mungu mahali pale: “Yeye [Mungu] hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu, Na kuutundika ulimwengu pasipo kitu” (26:7). “Nafasi isiyo na kitu” ya “kaskazini” huafikiana na kile ambacho wanajimu wamekiona kuwa ni sehemu isiyo ya kawaida yenye upungufu wa nyota katika mwelekeo huo. Bila shaka, Shetani alimvamia Mungu katika mwelekeo huo wakati alipotafuta kujiinua kutoka kwenye kiti chake cha enzi ili kukikalia kiti cha enzi cha Mungu katika “pande za kaskazini.” Hiki ndicho Biblia inachokifunua!
Ezekieli 28
Ezekieli 28:12-17 huenda sambamba na hutilia mkazo Isaya 14, na ni muhimu nayo tukaisoma. Kifungu hiki kinaelezea kile ambacho baadhi ya “wasomi” hudai alikuwa mwanadamu “mfame wa Tiro.” Usomaji wa makini huonyesha hiki hakiwezekani—na ni upuzi.
Fungu hili huongelea juu ya mmoja ambaye “hutia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri,” ambaye pia “alikuwa ndani ya Edeni, bustani ya Mungu.” Hakuna mwanadamu aliyewahi kuwa mkamilifu, huyu alikuwa ni shetani—joka—aliyemdanganya Hawa pale Bustanini. Fungu la 13 husema, “katika siku ya kuumbwa kwako,” na Shetani ni kiumbe aliyeumbwa. Fungu la 14 humwita “kerubi afunikaye.” (Kutoka 25:17-20 huelezea “makerubi wawili waaminifu waliobaki wa[lio]funika” kiti cha enzi cha Mungu katika hema ya Agano la Kale. Mabawa yao hufunika “kiti cha rehema.”) Maelezo haya hayawezi kuwa ya mfalme yeyote wa kidunia.
Sehemu ya mwisho ya Ezekieli 28:14 inasema kwamba “mfalme” huyu alikuwa “katika mlima wa Mungu” na “alitembea…kati ya mawe ya moto.” Hii huelezea eneo linalozunguka kiti cha enzi cha Mungu. Fungu la 15 hutamka, “uovu [uvunjaji wa sheria] ulipoonekana ndani yako” na fungu la 16 linaurejelea kama “dhambi.”
Fungu la 16 pia humwelezea kerubi huyu kama aliyekuwa “ametolewa…nje ya” mbingu. Mungu pia alisema “angemwangamiza” (Kiebrania: fukuzia mbali) Nyota ya alfajiri kutoka mbinguni. Fungu la 17 hufunua kwamba “moyo wake uliinuka kwa sababu ya uzuri [wake]” na kwamba “hekima yake iliharibiwa… kwa sababu ya mwangaza [wake].” Fungu hili linamalizikia kwa Mungu “kumtupa chini,” mahali ambapo wafalme wa dunia wangepata “”kumtazama.”
Nyota ya alfajiri alikuwa ni kiumbe mwenye akili sana—“malaika wa nuru,” kama walivyo “watumishi wake” (2 Kor. 11:13-15). Jina Nyota ya alfajiri lina maana ya “mwenye kuleta nuru.” Kiumbe huyu aliyekuwa mkamilifu hapo awali alileta nuru ing’arayo kwa wote waliokuwa wakimzunguka. Lakini aliasi na kutenda dhambi—na hivyo kuwa “mkuu wa giza.” Uasi wake ukamgeuza kuwa kiumbe aliyepinda, aliyepotoka. Japokuwa ni mwenye akili nyingi, kwa hakika amekuwa malaika kichaa aliyeanguka, asiyejua kutofautisha jema na baya!
Mnyama na Nabii wa Uongo
Ufahamu wa ziada kuhusu unabii fulani nyeti, ambao haujatimia ni wa lazima kabla ya kuendelea na kile kilichomtokea Shetani alipotupwa duniani.
Watu wawili, wanaojulikana kama “mnyama na nabii wa uongo,” watauongoza mfumo wa mwisho wa kidini-na-kiselikali wenye nguvu ulioonyeshwa kwenye Ufunuo 17 na 18, ambao Kristo ataupondaponda na kuchukua mahala pake katika Kurudi Kwake. Ufunuo 16:13-14 huelezea roho za mashetani kama zikiwa na nguvu ya “kufanya miujiza” kupitia mfumo huu. Mnyama akiwa ndiye kiungo kikuu cha mfumo huu, atakuwa mtu mkuu atawalaye ulimwengu.
Nabii wa uongo naye, ataongoza ulimwengu kumwabudu mnyama kama Mungu (Ufu. 16:2; 19:20)! Udanganyifu huu utaenea sana (18:3)—kwa ukamilifu—kiasi kwamba watawadanganya wanadamu wote kufikia kupigana na Kristo katika Kuja Kwake Mara ya Pili (16:9, 13-16; 17:13-14)!
Sasa angalia 2 Wathesalonike 2:3-4 na 8. Fungu la 3 humrejelea yule anayeitwa “mtu wa kuasi” na “mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.” Nabii wa uongo naye pia hudai kwamba ni Mungu.
Linganisha hiki na Ezekieli 28:2 na kielelezo cha “mfalme wa Tiro”—mwanadamu. Ezekieli aliandika kwamba “mfalme” huyu husema “Mimi ni Mungu, naketi katika kiti cha Mungu,” 2 Wathesalonike 2:8 humwelezea huyu “mtu wa kuasi” kama “[yule] mwovu” ambaye “atafunuliwa” namna vile alivyo wakati Kristo anaporudi na kumwangamiza pamoja na mnyama katika ziwa la moto (Ufu. 19:20). Isaya 14:4 humrejelea nabii wa uongo kama “Mfalme wa Babeli.” Huyu ndiye yule yule “Mfalme wa Tiro,”
Ukiendelea katika 2 Wathesalonike 2, fungu la 9 hutoa kauli ya kushangaza juu ya nabii wa uongo. Inasema kwamba “kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo.” Fungu la kumi huonyesha kwamba anaweza kumdanganya kila mmoja “asiyependa kweli.” Fungu la 11 hufunua kwamba Mungu ataleta “nguvu ya upotevu” kwa wote ambao kwa utashi wao huamini uongo wake.
Viongozi wa mfumo huu mkuu wa uongo watakuwa wamepagawa moja kwa moja na shetani! Hali hii itampatia nabii wa uongo nguvu nyingi sana za kudanganya na kutenda miujiza. Shetani, ambaye wakati wote ametamani kumpindua Mungu na kuchukua mahali pake, atanena kupitia mtu huyu ambaye ni kiongozi wa kidini na kuutangazia ulimwengu wote kwamba, hakika yeye ni, MUNGU! Onyo hili la Biblia halina utata. Miujiza atakayotenda itawadanganya walio wengi sana miongoni mwa watu!
Je, utadanganywa wakati matukio haya yatakapoanza kutokea hivi karibuni—maana hakika yatatokea? (Soma kijitabu chetu Nani au ni Nini Mnyama wa Ufunuo? Kujifunza zaidi juu ya huyu kiongozi wa mwisho wa ulimwengu.)
Alitupwa Hata Nchi na Malaika Zake Wote
Ufunuo 12 husema juu ya Shetani na pepo wake wabaya “walitupwa katika nchi” (fu. 13). Kwa hakika sura hii imepachikwa katikati ya kitabu cha Ufunuo, na ni muhtasari mfupi wa historia ya Kanisa la Agano Jipya.
Fungu la 3 linamwelezea Shetani kama “joka” aliye “kokota theluthi ya nyota za mbinguni na kuziangusha katika nchi” (fu. 4). Kumbuka kwamba “nyota” hizi zilikuwa ni theluthi ya malaika wote waliokuwa chini ya Nyota ya alfajiri kabla hajaasi.
2 Petro 2:4 hutoa kiashiria kingine juu ya huku “kutupwa chini” kwa Shetani na malaika zake “aliowakokota pamoja” naye. Angalia: “Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa [Shetani hakuwa malaika pekee aliyeasi], bali aliwatupa shimoni.” (Neno la Kigiriki hapa ni tartaros na linamaanisha aidha “gerezani” ama “kizuizini”—hii ni dunia yenyewe.) Pepo hawa wabaya pamoja na Shetani “wanalindwa hata ije hukumu,” wakiisha “kutiwa…katika vifungo vya giza.” Hii inafunua kwamba Mungu aliwatia katika gereza hili la giza pepo wengine wengi walioanguka waungane na “mkuu wa giza.”
Ufunuo 12:7-9 hueleza, kwa undani, lini Shetani na pepo wake wabaya watatupwa hata nchi kwa mara ya mwisho wasipate tena kibali cha kuingia mbinguni. Mafungu ya 12-14 yanaonyesha kwamba mwitikio wa ibilisi ni hasira kuu. Wakati huu wa kutisha unakuja kwa ulimwengu mzima hapo mbeleni kidogo!
Hatima ya Shetani
Lakini kitatokea nini kwa Shetani mara baada ya Kurudi kwa Kristo? Je, ataachwa huru kurandaranda duniani, akiendelea “kudanganya” (Ufu. 12:9) na “kudhoofisha” (Isa. 14:12) mataifa? Je, ataruhusiwa kubakia kuwa “mungu wa ulimwengu huu” (2 Kor. 4:4) milele? Hatima yake ni nini?
Ufunuo 20 huelezea Kristo akisimamisha utawala wa milenia kwa miaka-1000 (fu. 4) na kuzileta “sura za mwisho” katika kisa cha Shetani. Fungu la 2 husema kwamba malaika mwenye nguvu (fu. 1) anamfunga hakika kwa “miaka elfu” na “kumtupa katika kuzimu,” mahali “anapofungwa.” Kisha malaika huyu “[hu]tia muhuri juu yake, kwamba asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie: na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.”
Paulo alitaja wakati wa Shetani kufungwa aliposema, “naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi” (Rum. 16:20). Hii ni ahadi ya Mungu kwa Wakristo wote wa kweli na wanadamu wote, kwa sababu Shetani amewatesa Wakristo na kawadanganya wanadamu kwa maelfu ya miaka!
Mtume Yuda alisema kwamba Shetani na pepo wake wabaya watatupwa nje ya mifumo ya sayari kwenda mahali ambapo Biblia hupafafanua kuwa hapana nuru. Fungu la 13 huwaongelea viumbe hawa wenye kudhalilika kama “nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliyowekewa milele.” Yule “mkuu wa giza” na malaika zake watapata kile wanachostahili—kile walichojiletea wao wenyewe. Yule ambaye hapo awali alijulikana kama “aletaye nuru” alichagua giza. Mungu atampatia giza kamili kwa muda wote utakaofuata!
Uwezekano Wako Mkuu
Waebrania 2:5 huelezea dunia chini ya “utawala wa malaika [halisi]” sasa, lakini inaweka wazi kwamba malaika hawa hawataendelea kuutawala “ulimwengu ujao.”
Mafungu ya ziada katika sura hii hufafanua kile kitakachotokea wakati malaika walioanguka wanaotawala ulimwengu huu sasa watakapoondolewa na mahali pao kuchukuliwa: “Mwanadamu ni nini hata umkumbuke?…Umemfanya mdogo punde kuliko [maelezo ya ziada: chini ya] malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima… Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake” (fu. 6-8).
Yakiongelea juu ya Kristo, mafungu ya 9-10 huendelea, “ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa…akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso.”
Je, ulishika—kamata—kile kilichosemwa? Mafungu haya yamebeba ahadi ya uwezekano wa kuduwaza unaopatikana kwako na kwangu. Wakristo wameitwa kurithi “vitu vyote” na wapate “kuvikwa taji ya utukufu na heshima,” vilivyoahidiwa kwao kutokana na mwito wa Mungu na dhabihu ya Kristo—“kiongozi mkuu wa wokovu wao.”
Hakuna utata kuhusu nini maana ya “vitu vyote”. “Hakuna kitu” (fu. 8) kitakachowekwa kando katika urithi huu. (Soma vijitabu vyetu vya bure Nini Thawabu Yako Katika Maisha Yajayo?, Ufalme wa Mungu ni Nini? na Hivi Wokovu ni Nini?, miongoni mwa vingine, kujifunza zaidi juu ya uwezekano wa kushangaza unaowangojea watakatifu wote wa kweli wa Mungu.
Katika Mathayo 4:9, Shetani alimwahidi Kristo utawala juu ya “vitu vyote” kama “angeanguka chini na kumsujudia.” Wakristo wameahidiwa utawala juu ya “vitu vyote” hivyo hivyo—lakini kwa sharti pekee kwamba wamwabudu Mungu wa kweli!
Shetani Afunuliwa
Herbert W. Armstrong alihitimisha kijitabu chake Je, Mungu Aliumba Shetani? na:
“Mungu alimweka kerubi mkuu, Nyota ya alfajiri, kusimamia serikali Yake duniani, lakini Nyota ya alfajiri alikataa kutekeleza mapenzi ya Mungu, amri za Mungu, serikali ya Mungu. Alitaka kuibadili na ya kwake mwenyewe. Hivyo akajiondolea sifa yeye mwenyewe.
“Adamu alikuwa na nafasi ya kutwaa mahali pake. Katika kinyanganyiro cha kuona kama Adamu angeshinda, kama angemtii Mungu, alishindwa. Badala yake alimtii ibilisi, na mwanadamu akawa mali ya ibilisi, na tangu hapo jamii yote ya binadamu ikawa imeuzwa kutelemkia mtoni kwa ibilisi.
“Yesu Kristo akaja miaka 4,000 baadaye na akaingia katika shindano hilo kubwa—shindano la kujaribiwa pale Mlimani. ALIKATAA kumtii ibilisi. Alinukuu maandiko kwa usahihi. Alimtii Mungu.
“Hatimaye, Alimgeukia ibilisi, na akampa Shetani amri. Alisema ‘Nenda zako Shetani,’ na ibilisi akatii!
Kutoka wakati huo na kuendelea, mrithi wa Shetani alifuzu kuchukua utawala wa dunia. Lakini Yesu alienda mbinguni kwa miaka 1,900. Atarudi tena hivi karibuni, na atakaporudi, ibilisi ATAONDOLEWA KUTOKA MAHALI PAKE. Kristo ataitawala dunia, Amri za Mungu zitarejeshwa. Hatimaye mpango sahihi na amani vitakuja!
“Kwa hiyo Mungu HAKUUMBA ibilisi. Aliumba kerubi, Nyota ya alfajiri—mkamilifu katika njia zake, lakini akiwa na nguvu ya uchaguzi huru—na Nyota ya alfajiri alijigeuza mwenyewe akawa shetani kwa kuasi Serikali ya Mungu!’
Tags
Michezo na Burudani