Ni hatari kwa afya ya watoto
SODA ni kinywaji kinachopendwa sana na watoto, kutokana na ladha yake tamu. Watoto ni miongoni mwa wanywaji wakubwa wa kinywaji aina ya soda. Wazazi wengi wanapotaka kuwafurahisha watoto wao huwanunulia soda bila kufahamu ina madhara yapi mwilini mwao. Katika sehemu ya pili ya makala hizi zinazotazama madhara ya soda kupitia tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa afya duniani, tutaangalia madhara ya soda kwa watoto wadogo.
Soda ina madhara kwa watoto kwa kuwa ina kemikali inayofahamika kitaalamu kwa jina la Caffeine. Caffeine ni aina ya kemikali inayozalishwa kwenye majani na mbegu za baadhi ya mimea. Caffeine pia huweza kutengenezwa na kuongezwa kwenye baadhi ya vyakula.
Kemikali hii ni hatari kwa kuwa huingilia mfumo wa fahamu na hivyo kufanya ushindwe kufanya kazi kama inavyotakiwa. Kwa upande mwingine Caffeine inaelezwa kuwa ni kilevi. Mtumiaji wa caffeine huchangamka na hupenda kuitumia mara kwa mara.
Baadhi ya madhara ya Caffeine iliyopo kwenye soda kwa watoto, ni pamoja na kumfanya mtoto kushindwa kufuatilia vizuri mambo ikiwa ni pamoja na masomo awapo darasani, kukosa usingizi pamoja na kuongezeka kwa mapigo ya moyo.
Utafiti uliofanywa na madaktari nchini Marekani na kuchapishwa katika jarida maarufu linalohusu afya kwa watoto la Journal of Pediatrics, unaonyesha kuwa watoto wenye umri kati ya miaka 5 hadi 7 wanaokunywa kinywaji cha soda chenye Caffeine, hulala masaa machache zaidi ya wale ambao hawatumii kinywaji chenye Caffeine.
Matokeo ya utafiti huo, yanaonyesha kuwa usingizi wa mtoto anaopata, huathiriwa na unywaji wa soda zenye Caffeine.
Tafiti nyingine zinaonyesha kuwa Caffeine ina madhara mengine zaidi kwa afya za watoto.
Utafiti uliochapishwa kwenye Jarida la Experimental and Clinical Psychopharmacology, unaonyesha kuwa unywaji wa kiasi kikubwa wa soda zenye Caffeine, husababisha kuongezeka shinikizo la damu kwa watoto wa kiume.
Watoto ambao hunywa soda kiasi cha milimita 355 kwa siku, wapo katika hatari ya kupata uzito mkubwa na kuongezeka kwa mafuta mwilini.
Vinywaji vingi vyenye Caffeine vina Kalori zisizo na kirutubisho chochote na hivyo watoto wanaovitumia vinywaji hivyo hukosa virutubisho muhimu kwa ajili ya ukuaji na maendeleo yao ya kiafya.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa, watoto wanaokunywa soda kwa wingi (kuanzia miaka 3 hadi 8), wapo katika hatari ya kukosa Madini ya Calcium, yanayopatikana kwenye maziwa ambayo husaidia kujenga uimara wa mifupa na meno.
Tafiti nyingine zinaonyesha kuwa, unywaji wa vinywaji vyenye sukari nyingi na hasa soda ni moja kati ya sababu kuu zinazosababisha kuoza kwa meno ya watoto wakiwa bado wadogo. Ikumbukwe kuwa kiwango cha sukari kilichopo kwenye milimita 355 za soda, ni sawa na vijiko kumi vya sukari.
Caffeine huongeza uwezekano wa watoto kupata magonjwa ya moyo na matatizo katika mfumo wa fahamu, jambo ambalo wazazi hawafahamu.
Pia, kuna baadhi ya ushahidi unaoonyesha kwamba, kama una mtoto ambaye tayari ana ugonjwa wa wasiwasi (anxiety disorder), madhara ya Caffeine humfanya kuwa na hali mbaya zaidi.
Wataalamu mbalimbali waliobobea katika masuala ya afya ya umma, wanaeleza kuwa madhara ya Caffeine kwa afya ya watoto iliyopo katika soda yana athari mbaya kwa watoto.
Dk. Marcie Schneider, daktari wa watoto na mmoja wa wanakamati wa Shule ya Afya ya watoto kwenye masuala ya lishe (American Academy of Pediatrics committee on nutrition) anaeleza kuwa, Caffeine kufyonzwa tishu za mwili. Inaongeza kiwango cha mapigo ya moyo na pia huongeza shinikizo la damu.
Kwamba Caffeine husababisha mabadiliko ya joto la mwili wa mtoto, husababisha mabadiliko ya namna mtoto alivyo na kusababisha usumbufu wakati wa usingizi.
Anaielezea Caffeine kuwa humchangamsha na husababisha msisimko usio wa kawaida na pia hubadili hamu ya kawaida ya kula. Vijana wanaochipukia hupata nusu ya uzito wao wa kiutu uzima wakiwa katika umri huo. Wakiathirika na Caffeine, ulaji wao mdogo huchangia kurudisha nyuma ukuaji wao.
Dk. Nicole Caldwell, Profesa msaidizi wa afya ya watoto katika Hospitali ya Taifa ya Watoto (Nationwide Children's Hospital) Columbus, Ohio, yeye anaeleza katika utafiti wake kuwa Caffeine huathiri mfumo wa fahamu ikiwa kama stimulant.
Ubongo wa mtoto ni rahisi zaidi kuathiriwa na Caffaine tofauti na wa mtu mzima, kwa sababu humfanya mtoto kuchangamka kupitiliza. Inaweza kuwasababishia wasiwasi, matatizo ya tumbo na matatizo ya usingizi.
Caffeine husababisha kusinyaa kwa mishipa ya damu. Inachukua miligramu 4 za Caffeine kwa kilo moja ya uzito wa mwili kuongeza shinikizo la damu.
Ushahidi hauonyeshi kuwa Caffeine inasababisha kudumaa, lakini watoto wanaokunywa vinywaji vyenye Caffeine wana nafasi ndogo ya kupata Madini ya Calcium, inayohitajika mwilini.
Lakini pia, kama mtoto anayekunywa soda yenye caffeine atakuwa anaingiza kiasi kikubwa cha sukari mwilini, ambacho huweza kusababisha kuoza kwa meno pamoja na kuongezeka uzito.
Ann Condon-Meyers, mtaalamu wa masuala ya chakula na lishe (a registered dietitian) katika hospitali ya Pittsburgh, yeye anaeleza kuwa ni stimulant, hivyo ni kama kilevi.
Uzito wa mtoto hueleza ni kiasi gani cha Caffeine mwili wake unaweza kuhimili. Kwa mfano mtoto mwenye uzito wa pauni 60 anaweza kuhimili miligramu 60 za Caffeine katika kipindi cha masaa 24. Tatizo ni kuwa kuna baadhi ya vinywaji vina kiasi kikubwa sana cha Caffeine.
Madhara yake ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha mapigo ya moyo, kuongezeka kwa shinikizo la damu, kuongezeka wasiwasi na upungufu wa uwezo wa kulala pamoja na homa.
Matatizo mengi yanayosababishwa na vinywaji hivi vyenye Caffeine husababishwa na kiasi kikubwa cha sukari kinachoongezwa kwenye vinywaji hivyo. Vinywaji hivi havina manufaaa yoyote kwa vile havina virutubisho. Unapokuwa na mtoto anayekunywa zaidi ya soda moja kwa siku, ujue yupo katika hatari ya kuongezeka uzito.
Mtoto anapoongezeka uzito usio wa kawaida (obesity) akiwa katika umri wa kuendelea kukuwa, anakuwa kwenye nafasi kubwa ya kuwa na tatizo hilo hata anapokuwa mtu mzima.
Unywaji wa vinywaji vyenye Caffeine haukukuwa na kujengeka kama tabia ya mtu. Binafsi napinga makampuni ya soda kutangaza bidhaa zao kwa watoto kwa kuwa si salama kwa afya yao. Nadhani ni wajanja kuweka Caffeine kwenye vinjwaji vyao kwa kuwa humfanya mtu kuwa kama teja ambaye huwaza kupata kinywaji hicho kila mara na hivyo ni kama kilevi.
Dk. Matthew Keefer, Mtaalamu wa Chakula na Lishe wa hospitali ya watoto huko Los Angels nchini Marekani, anaeleza kuwa Soda haina shida sana, lakini ina madhara mengi yasiyo ya lazima.
Anasema watoto wadogo hawahitaji Caffeine hata kidogo. Kama mtoto mwenye umri wa kati akipata kikombe cha kahawa au soda mara chache siyo jambo baya. Lakini kwa watoto wadogo huweza kusababisha kupoteza maji mengi mwilini.
“Tunatumia Caffeine kwa watoto wachanga kama wanakuwa na matatizo ya kukumbuka kupumua. Mara chache hutumika kwa watu wenye homa ya migraine, lakini zaidi ya hapo haina matumizi mengine ya kitabibu,” anaeleza Dk. Keefer.
Lakini pia inaelezwa kuwa kuna sababu kwa nini Caffeine iliyo kwenye mfumo wa kahawa ina bei ndogo. Imepewa ruzuku na makampu
ni makubwa na hivyo kuuzwa kwa bei ndogo sana.
Sababu hiyo ni kuwafanya wafanyakazi wawe wachangamfu na wenye kufanya kazi bila kuchoka. Lakini kwa watoto ni tatizo kwa sababu huwapunguzia muda wa kupumzika wakati bado wanahitaji kukuwa.
Watoto wanahitaji kulala usingizi wa kutosha. Huhitaji masaa 8 au 10 kulala usingizi wakati wa usiku, lakini wanapotumia vinywaji vyenye Caffeine hupata usingizi wa kutosha kwa shida.
Tags
Jiwe la wiki