UTANGULIZI
KIJITABU hiki ni mkusanyiko wa mawazo,
dira, muongozo na ramani halisi juu ya baadhi ya mambo yatakayofanyika jimboni
Manonga. Nasema ni baadhi kwa sababu haya ni mawazo yangu binafsi kama mbunge,
endapo wananchi watanipa ridhaa ya kuwawakilisha tena Bungeni kwa miaka mingine
mitano ijayo.
Mawazo yangu haya, pia yatanakishiwa
na mawazo ya wananchi wa Jimbo letu la Manonga, wanayopenda kufanyiwa na
Serikali yao sikivu inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Maana yake ni kwamba, nitayachukua
mawazo yao na kuyaweka pamoja na haya kwangu ili nibebe zana nzima ya mahitaji
ya Wanamanonga.
Mjumuiko wa Dira hii unatokana pia na
kuchukua baadhi ya ajenda zilizomo kweye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi,
inayoeleza mambo mengi yanayotarajiwa kufanywa na Serikali itakapoingia tena
madarakani kwa mwaka 2020-2025.
Hivyo basi, mchanganyo wa
kilichoandikwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM na mchanganuo wa mawazo
yangu binafsi ndivyo vimezaa Dira hii ya awali ambayo itakamilika baada ya kukusanya
pia mawazo ya wananchi ambayo pengine wangependa kufanyiwa na Serikali pindi
itakapoingia madarakani, ndiyo maana nasema hii ni Dira ya awali.
Binafsi nichukue nafsi hii kukipongeza
sana chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuikumbuka Barabara za Puge
hadi Ndala na Ziba hadi Choma ambazo kwa ujumla zina Km 83 na kuziingiza kwenye
utekelezeaji wa miradi ya barabara iliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka
huu. Ninashukuru sana.
Imani yangu ni kwamba, yote
niliyoainisha kwenye Dira yetu hii yatakamilika katika katika kipindi chote cha
miaka mitano ya uwakilishi wangu kama Mbunge wa Jimbo la Manonga.
Naomba nieleweke, katika kuyakamilisha
yote haya ni mjumuisho wa miaka mitano, isije ikatokea ukapita mwaka mmoja,
miwili au mitatu watu waanze kudai ahadi hizi, ndiyo maana ninasisitiza ni
utekelezaji wa miaka yote mitano ijayo uanzia pale nitakapoapishwa tena
kuliwakilisha jimbo langu ninalolipenda sana la Manonga.
KALAMU YANGU
Mimi Seif Khamis Said Gulamali,
ninawiwa mno moyoni mwangu kutoa shukrani za dhati kwa chama changu, Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwa kuwa na Imani na mimi na kunipitisha tena kwa ngazi zote,
kuanzia wajumbe na hatimaye Mkutano wa Halmashauri Kuu. Hakika sina cha
kuwalipa zaidi ya kusema ninashukuru mno na Mungu ni shuhuda wa hisia za
shukrani hizi kutoka kwenye uvungu wa moyo wangu.
Pia, ninazo shukrani za dhati kwa
wananchi na wakazi wa Jimbo letu la Manonga kwa kuniachagua kwa kishindo katika
uchaguzi wa mwaka 2015 na sasa ninayo Imani na matarajio makubwa kwao kwamba
watafanya zaidi ya ilivyokuwa mwaka 2015.
Sina cha kuwalipa zaidi ya kuwapigania
maendeleo. Nitahakikisha ninajitoa kikamilifu kuwatetea, kuwasemea na
kuwawakilisha kwa kila njia iliyo njema na halali kwa Serikali na Mungu anijalie
hekima katika kuyatimiza majukumu yangu ya kibunge. In-shallah.
DIRA INAVYOELEZA
Dira hii imegawanyika katika vipengele
tofautri kutokana na huduma za kijamii. Nayo ni kama ifuatavyo;
(i)
KILIMO NA UFUGAJI
(a)
Kilimo
Kwa kutambua kuwa
kazi na shughuli kuu za uzalishaji zinazofanywa na wakazi wa Jimbo la Manonga
ni kilimo na ufugaji, mimi kama Mbunge mtarajiwa (ninaamini itakuwa hivyo),
nimelazimika kuwa na mawazo na fikra chanya zaidi katika kuhakikisha kilimo na
ufugaji vinafanyika kwa njia bora tena za kitaalamu ili kutoa tija halisi kwa
wakulima na wavuvi.
Katika kuzingatia hilo, nitahakikisha
ninahamasisha kilimo cha kisasa kwa kuleta wataalum kutoka taasisi mbalimbali
za kilimo na ufugaji ili kutoa elimu stahiki kwa wakulima ili kujipatia mazao mengi
yenye kukidhi mahitaji ya chakula na biashara.
Pia kuweka mazingira bora ya soko la
mazao ya biashara hususan Pamba ikiwa ni pamoja na unafuu wa pembejeo za kilimo
hicho na malipo halali tena kwa wakati na hatimaye kuinua kipato na uchumi wa
wakazi wa Jimbo la Manonga.
(b)
Ufugaji
Kwa kuzingatia sera ya kisasa ya
ufugaji wa kitaalam, pia ninayo mawazo na mpango wa kuhamasisha ufugaji bora wa
mifugo mbalimbali ikiwemo ufugaji wa kisasa wa samaki, ambapo ukweli ni kwamba
ufugaji wa kisasa wa samaki umekuwa kiinua uchumi kwa Watanzania wengi, ukilinganisha
Kijiografia Jimbo la Manonga ambalo lipo mkoani Tabora halipo mbali na vyanzo
vikuu vya samaki ambavyo ni Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika pamoja na mabwawa
mengine makubwa.
(ii)
UJASIRIAMALI
Katika kutimiza na kuendeleza matokeo
haya ya kipato cha kati ambacho nchi yetu imefikia hivi karibuni, nimebuni
mpango wa kuwawezesha vijana na akina mama kijasiriamali, ambapo
nitawakutanisha kila kata na kuleta wataalam wa elimu ya ujasiriamali ili kutoa
mafunzo mbalimbali ya utengenezaji wa bidhaa yenye uhitaji mkubwa katika jamii
Mfano; wa bidhaa hizo ni kama sabani
za maji, sabuni za miche, vitenge vya batiki, pilipili, mvinyo (wine), upishi
wa kisasa na kadhalika.
Mafunzo haya yatawasaidia akina mama
na vijana kuweza kujikwamua kiuchumi na kipato kwao binafsi na kwa taifa
kupitia malipo ya kodi.
(iii)
ASASI BINAFSI YA MIKOPO NAFUU-
MANONGA DEVELOPMENT COOPERATION (MADECO)
Serikali kuanzia mwaka 2015-2020
iliweza kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa vikundi mbalimbali vya vijana na
akina mama, ambapo zaidi ya vikundi 3,035 katika mikoa yote 26 ya Tanzania bara
viliwezeshwa kwa Benki ya Posta (Tanzania Postal Bank) kutoa zaidi ya Sh.
Billioni 2.05 na pia Halmashauri zote 185 kutoa Sh. Billioni 93.3 kwenye mfuko
wa kuwawezesha wanawake, vijana na wenye ulemavu vikundi vipatavyo 32,553.
Katika kuzingatia na kuendeleza zana
ya uwezeshaji kwa wanawake, ijana na watu wenye ulemavu, nimebuni kuanzisha
asasi binafsi itakayomilikiwa na wakazi wa Jimbo la Manonga, yenye udhamini wa
Mbunge.
Asasi hiyo itatumika kama asasi
zingine zisizokuwa za kiserikali kuomba mikopo yenye masharti nafuu na kutoa
kwa wanachama husika, ili waweze kutumia katika kuendesha miradi mbalimbali ya
kimaendeleo na kurejesha riba kwa masharti nafuu na muda usioumiza mkopaji.
(iv)
MIUNDOMBINU
Kuhusu miundombinu ya barabara na
madaraja, ninamshukuru sana Mungu na Serikali yetu kuwezesha ujenzi wa daraja
la Mto Manonga, daraja ambalo kwa hakika lilikuwa kilio cha wakazi wa Manonga
kwa myda mrefu.
Sasa ukamilikaji wa ujenzi wa daraja
hilo umerahisisha usafiri kutoka Manonga hadi mkoani Shinyanga kwa kupunguza
wingi wa Kilomita. Hii si tu kwa wakazi wa Manonga bali imekuwa nafuu kwa
Watazania wengi wanaosafiri kupitia barabara hiyo.
Pia katika Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi ya uchaguzi wa mwaka huu, barabara za Puge hadi Ndala na Ziba hadi
Choma zimo katika mpango wa kutengenezwa, jambo ambalo siyo tu kwamba
litarahisisha usafiri wa watu lakini pia usafirishaji wa mazao wakati wa
mavuno.
Hivyo, mimi kama mbunge kwa niaba ya
wananachi wenzangu wa Jimbo la Manonga, ninatoa shukrani za dhati kwa Chama Cha
Mapinduzi na Serikali yake kwa ujumla kwa kuzikumbuka barabara hizi zenye jumla
ya urefu wa Kilomita 83.
Nami nimejipanga kuendeleza ubunifu wa
barabara ambazo zinaelekea kwenye huduma za kijamii ambazo hakuwepo tangu
kuumbwa kwa misingi ya dunia, kama ambavyo nilifanya baada ya uchaguzi wa mwaka
2015.
(v)
NISHATI
Katika hili, pia niishukuru sana
Serikali kwa kutekeleza sera ya uwashaji wa umeme vijijini kupitia ule mradi wa
Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Wakati naingia kwenye nafasi ya
uwakilishi kama Mbunge mwaka 2015, Jimbo la Manonga lilikuwa gizani karibu nusu
au zaidi ya kata zake zote pamoja na vijiji.
Lakini leo ndani ya miaka mitano ya
Ubunge wangu tumewezesha kupeleka umeme kwenye kata 18, ambapo jimbo letu lina
kata 19, hivyo ni kata moja tu ambayo bado haijamalizwa lakini ipo katika
mpango kabambe wa kuwashwa umeme.
Kwa hiyo lengo langu Katika hili ni
kuishauri na kuiomba Serikali imalizie mpango wake wa kuwasha umeme katika
vijiji vyote vya kata hiyo moja iliyosalia.
(vi)
MADINI
Jimbo letu la Manonga, pia
limebarikiwa kuwa na migodi midogo ya uchimbaji wa madini.
Katika kuhakikisha migodi hii inaleta
tija kwa wakazi wa Jimbo la Manonga, mimi kama Mbunge nimehamasika kuwawezesha
wachimbaji wadogowadogo kwanza kupata leseni za uchimbaji na kuwa na vitendea
kazi bora ili waweze kurahisisha shughuli zao za uchimbaji wa madini.
Lakini pia katika hilo, ni kuwawezesha
kuyafikia kwa urahisi masoko ya madini ambayo kwa sasa yapo maeneo mengi nchini
kwetu katika maeneo ambayo yana uchimbaji wa madini.
(vii)
HUDUMA ZA KIJAMII
(a)
Elimu
Katika kipindi cha miaka mitano ya
uwakilishi wangu wa Ubunge katika Jimbo la Manonga, nimewezesha ujenzi shule za
sekondari takribani sab ana kuvuka lengo la awali, hivyo ni hatua nzuri ya kuhakiksha
tunauwa na miundombinu bora ya kielimu katika Jimbo letu la Manonga.
Pia, nimewezesha ujenzi wa vyumba vya
madarasa kwa ajili ya shule ya Elimu ya kidato cha tano na sita katika shule za
sekondari za Ziba na Mwisi, ambapo vijana wetu wanakuwa na mazingira rahisi ya
kupata elimu ya kidato cha tano na sita.
Vilevile katika kuhakikisha tunawainua
na kuwatia nguvu vijana wetu, mimi kama Mbunge kwa kutoa fedha yangu ya
mfukoni, nimewezesha kusomesha Watoto ambao wamekuwa wakifaulu vizuri kutoka
kidato cha nne kwenda kidato cha tano na hata vyuo mbalimbali na Vyuo Vikuu.
Leng langu kwa miaka mitano ijayo, ni
kuongeza idadi zaidi na hamasa kubwa katika kujenga shue zingine za kidato cha
tano na sita na pia kuendelea kuwasomesha vijana wetu wenye uwezo mkubwa
darasani lakini kwa miaka mingu wamekuwa wakikwamishwa na uduni wa maisha
kutoka kwa familia zao hivyo na kushindwa kufikia malengo na ndoto zao za
kimaisha.
Pia, katika kuhamasisha ukuaji wa
elimu kwa Jimbo la Manonga, nimebuni kuanzisha mashindano ya kitaaluma kwa
shule zote za msingi na sekondari, ambapo wanafunzi wa Darasa la Nne watakuwa
na mashindano yao kabla ya kufanya mtihani wa Taifa kwa kujiunga na Darasa la
Tano.
Pia wanafunzi wa Darasa la Saba
watakuwa na mashindano ya kitaaluma kabla ya mtihani wa kujiunga na Kidato cha
kwanza.
Wanafunzi wa Kidato cha Pili watakuwa
na mashindaho ya kitaaluma kabla ya mtihani wa kujiunga na Kidato cha Tatu na
wanafunzi wa kidato cha Nne watakuwa na mashindano hayo kabla ya mtihani wa
kujiunga na Kidato cha Tano na hata wanafuzi wa Kidato cha Sita wakakuwa na
mashindano hayo kabla ya mtihani wa Taifa wa kujiunga na Elimu ya Chuo Kikuu.
Mashindabo hayo yataitwa Gulamali
Academy Rise Competition (GARICO)
(b)
Afya
Kuhusu sekta ya Afya, ninashukuru
Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Simbo kama nilivyoahidi
kufanya na vilevile kutoa mchango wangu binafsi katika ujenzi na kuleta gari la
wagonjwa, gari la kisasa kabisa lenye hadhi kubwa.
Lengo langu ni kuhakikisha tunakuwa na
vituo vingine vya Afya angalau viwili au
vitatu katika Jimbo letu la Manonga ili kurahisisha huduma ya Afya.
Serikali imejitahidi sana kujenga
zahanati na Vituo vya Afya pamoja na Hospitali kila wilaya. Kuhusu zahanati,
mwaka 2015 zilikuwa 6,044 na leo ni takribani 7,242.
Kuhusu Vituo vya Afya, vilikuwa 718 na
leo mwaka 2020 ni vituo vya Afya vipatavyo 1,205.
Pia ninao mpango kama Mbunge wa
kusaidi upatikanaji wa Bima za Afya kwa watu wenye ulemavu, Watoto yatima na
hata wajane ni wazee na hawana walezi.
Pia, suala la Bima la Afya itakuwa ni
hamasa kwa wakazi wote wa Jimbo la Manonga ambao wanapaswa kupewa elimu ya kuwa
na Bima ya Afya ambayo imekuwa ikitolewa kwa bei nafuu kutoka Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF).
(viii)
MAJI
Kuhusu sekta ya maji, tumeshuhudia
uvutwaji wa maji kutoka ule mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambayo tayari
yanatumika kwa baadhi ya maeneo jimboni Manonga na Igunga mjini. Kama ambvyo
Mhe. Rais Dkt. Magufuli alivyoahidi kuleta zaidi ya hapo. Lakini pia katika
hili linedhamiria kusisitiza bei nafuu kwa wakazi wa Manonga ili waweze kupata
huduma ya maji haya kwa unafuu zaidi.
Pia, nimejipanga kuwezesha uchimbaji
wa visima vya kudumu katika maeneo kadhaa ya Jimbo la Manonga ili kurahisisha
huduma hii muhimu kwa wananchi wa Jimbo letu la Manonga.
(ix)
ULINZI NA USALAMA
Kama mtakumbuka, Rais Magufuli alisema
Ziba inafaa kuwa Wilaya hii ni kutoka na ongezeko la wakazi, ambao wanafuata
unafuu wa utafutaji wa riziki za maisha. Nimejipanga kuhamasisha na kuishauri
Serikali kuongeza vituo vya polisi katika meneo mengi yenye mkusanyiko wa watu
ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya askari polisi katika vituo vya Ziba na
Nkinga.
Pia, kuendela kuisisitiza Serikali
kutupatia Halmashauri yetu na Wilaya ili kurahisha huduma za kijamii kwa
watumishi na wakazi wengine.
(x)
UDHIBITI WA WIZI NA RUSHWA
Pia nimejipanga zaidi kudhibiti
maradufu wizi wa mali za umma. Kama mtakumbuka ujio wa Waziri Mkuu Ziba
ulipelekea kuwekwa ndani kwa mmoja wa viongozi kutokana na wizi na ubadhilifu
wa mali za umma. Hivyo, katika awamu ijayo, nimejipanda maradufu kudhibiti wizi
wa mali za umma pamoja na mazingira ya rushwa kwa watumishi wa huduma za jamii.
(X) MICHEZO
Kama mtakumbuka nimekuwa nikianzisha
mashindano mbalimbali ya michezo ikiwemo Gulamali Cup kwa wanakijiji na
wanafunzi. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, nimepanga kuanzisha klabu
kubwa ya michezo mbalimbali, iitwayo Manonga Sports Club.
Klabu hii itajumuisha timu ya mpira wa
miguu (Manonga FC) ambayo lengo ni kuifikisha Ligi Kuu, pamoja na kuendeleza
zaidi timu ya mpira wa miguu ya wasichana ya Manonga Queens pamoja na michezo
mingine.
HITIMISHO
Kaulimbiu yetu sisi Wanamanonga ni
Upendo, Bidii ya Kazi, Heshima na maendeleo. KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
Ni mimi ndugu yenu,
SEIF KHAMIS GULAMALI
2020-2025