KWANINI WAKATOLIKI HUPENDA KUPIGA ISHARA YA MSALABA NA JE KUPIGA ISHARA YA MSALABA MARA NYINGI WAKATI WA MISA NI HALALI?

 



Ndugu zangu Wakatoliki katika Bwana, natumaini mu wazima wa afya. Leo nimekuja na somo hili kwenu, ni kwa sababu wengi wetu hatujui maana wala umuhimu wa kupiga Ishara ya Msalaba. Pia tunadhani ya kwamba kupiga Ishara ya Msalaba mara nyingi wakati wa Misa ni sahihi, kumbe tunakosea.



Hivyo kabla sijaenda kwenye somo letu kuu la leo, napenda kwanza kuanza kwa kusema maneno yafuatayo:-


JE WAJUA NINI MAANA YA MSALABA?

- Msalaba ni alama hai ya upendo wa Yesu Kristo kwa kujitoa mwenyewe bila kujibakiza, ili kuweza kutukomba sisi wanadamu. Rej (Yoh 3: 16)


JE NINI SASA MAANA YA MSALABA WA YESU?

- Msalaba wa Yesu ni ule ambao Yesu mwenyewe alisulubiwa juu yake  huko Yerusalemu, kwa amri ya Ponsyo Pilato siku ya ijumaa, na inasemekana ilikuwa ni tarehe 7 April 30 B.K


JE KUPIGA ISHARA YA MSALABA MAANA YAKE NINI?

- Kupiga Ishara ya Msalaba maana yake ni:-

(a) Kukiri ukombozi wetu uliopatikana kwa njia Yesu Kristo pale juu Msalabani.


(b) Kukiri Utatu Mtakatifu. Yaani:-


- Mungu Baba alimtuma Mwanae toka Mbinguni, naye akashuka chini kutuokoa.

- Aliyetumwa duniani (Yesu Kristo), alituokoa na kututoa katika dhambi.

- Kisha akatuleta kwa njia ya Roho Mtakatifu kwenye wokovu.

- Mwisho tunasema "AMINA" maana yake, ni kuungama na kuliamini tendo hili la kufanya Ishara ya Msalaba, kama njia ya Ukombozi.


JE KUPIGA ISHARA YA MSALABANI KWENYE PAJI LA USO MAANA YAKE NINI?

- Ni kukubali kwa akili kuwa, bila Msalaba tusingepata Neema ya Wokovu.


JE KUPIGA ISHARA YA MSALABA KWENYE KIFUA MAANA YAKE NINI?

- Ni kupenda na kuupokea moyoni, kile ambacho Yesu alikifanya kupitia Msalaba.


JE KUPIGA ISHARA YA MSALABA KWENYE MABEGA MAANA YAKE NINI?

- Ni kuwa tayari kuubeba Msalaba kwa nguvu zako zote, bila kujali ugumu na changamoto za maisha.


JE ISHARA YA MSALABA KABLA YA INJILI MAANA YAKE NINI?

- Ishara ya Msalaba wakati wa Injili maana yake ni:-


(a) UTOSINI = Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu kwa akili yangu.

(b) MDOMONI = Nitalitangaza kwa ushujaa Neno la Mungu kwa kinywa changu.

(c) KIFUANI = Nitalipenda Neno la Mungu na kulishika moyoni mwangu maisha yangu yote.


JE KUNA AINA NGAPI ZA ISHARA YA MSALABA?

- Kuu aina kuu mbili (2) tu za Ishara ya Msalaba, nazo ni:-


(a) Ishara kubwa ya Msalaba

- Hii tunaifanya kila siku kabla na baada ya Sala.


(b) Ishara ndogo ya Msalaba

- Hii tunaifanya hasa zaidi wakati wa Injili kwenye Misa takatifu, Wakati wa Sakramenti ya Ubatizo na Mpako wa wagonjwa n.k.

- Na mara nyingi hupigwa kwa kutumia kidole gumba kimoja.


JE NJIA YA MSALABA MAANA YAKE NINI?

- Njia ya Msalaba maana yake ni tafakari ya Yesu tangu hukumu ya Pilato hadi alipozikwa kaburini.

- Husaliwa kila ijumaa katika kipindi cha Kwaresma.

- Pia ni tafakari nzito sana ya maisha ya kila siku ya mwanadamu, juu ya toba na kuongoka na sio kuokoka. Kisha kumfuasa Kristo kwa kutafakari mateso makali aliyoyapata, kwa ajili ya ukombozi wetu.


JE UMUHIMU WA MSALABA KATIKA MAISHA YA MKRISTO MKATOLIKI NI ZIPI?

- Kuna faida nyingi za Msalaba na kupiga Ishara ya Msalaba. Kwa uchache zaidi naweza kusema:-


1. Ni kitambulisho cha Ukatoliki wetu.

2. Tunakiri uwepo wa Mungu katika Nafsi tatu.

3. Ni kinga yetu dhidi ya shetani.

4. Huleta uponyaji wa kiroho na wa kimwili pia.

5. Ni dawa dhidi ya laana na magonjwa.

6. Ni ishara ya unyenyekevu katika kujikabidhi kwa Mungu hasa wakati wa sala.

7. Ni ukumbusho wa wokovu wetu.


N:B = Kwa kupigwa kwake, sisi sote tumepona. Rej (1Pet 2:24)


Baada ya kuangalia maana ya Ishara ya Msalaba na umuhimu wake. Sasa turudi kwenye wazo letu kuu:


JE KUPIGA ISHARA YA MSALABA MARA NYINGI WAKATI WA MISA NI HALALI?

- Kupiga Ishara ya Msalaba mara nyingi wakati wa Misa ikiendelea, sio halali na hairuhusiwi.


- Daima tunapaswa kupiga Ishara ya Msalaba mara mbili (2) tu, yaani kabla ya Misa kuanza na baada Misa kuisha.


SWALI: JE NI KWA SABABU GANI?

- Mama Kanisa anatufundisha kuwa:


• Hatutakiwi kufanya Ishara ya Msalaba wakati wa Misa ikiendelea, hasa kwenye ungamo la dhambi, pale Padre anaposema: "Mungu Mwenyezi atusamehe dhambi zetu, atufukishe kwenye uzima wa milele"


KWANINI? Ni kwa sababu, sala hiyo sio ya kuwabariki waamini wala sio tendo la kuondolea dhambi, kama ilivyo Sakramenti ya Kitubio.


• Hivyo tendo hilo ni kutafakari dhambi zetu na kutubu pamoja. Maana linatusaidia kujiona tu wakosefu, na kwa unyenyekevu tunakiri hali yetu ya dhambi mbele za Mungu, kwa kumtolea sadaka ya Yesu Kristo Mwanae.


• Pia hatutakiwi kufanya Ishara ya Msalaba wakati wa Consecrasio, pale Kuhani anaposema: "Tunakusihi ee Bwana, upokee vipaji hivi..."


KWANINI? Hapa Padre anabariki Maumbo ya Mkate na Divai, kuwa Mwili na Damu ya Yesu, na sio wewe kujibariki kwa kupiga Ishara ya Msalaba.


• Nafasi nyingine ni mwanzo wa Homilia. Hapa baadhi ya Makuhani huanza Homilia kwa kutaja wazo kuu la Homilia, halafu hujiandika Ishara ya Msalaba, na waamini wakimuiga. Haitakiwi.


KWANINI? Ni kwa sababu kufanya ishara ya Msalaba ni kama kuanza jambo jipya. Homilia sio kitu cha kusimama peke yake, bali ni sehemu ya Liturjia ya Neno.


• Mbaya zaidi wengine humaliza Homilia kwa Ishara ya Msalaba na kupiga makofi kwa madoido, vigelegele n.k.


• Hayo yote hayatakiwi wakati wa Injili, bali tunatakiwa kukamilisha Homilia kwa tafakari katika ukimya, na sio kwa makofi wala kupiga vigelegele hata kama mahubiri ya siku hiyo yamekuvutia. Kwa kuwa unapofanya hivyo, unaharibu tafakari.


• Tena wakati wa kupeleka vipaji, mara nyingi Padre huwa anapenda kufanya Ishara ya Msalaba. Lakini cha ajabu wakati wa tukio hili, waumini wote humuiga Padre kwa kupiga Ishara ya Msalaba.


• Ukweli ni kwamba, wanaoruhusiwa kupiga Ishara ya Msalaba ni Jumuiya husika wanaohudumia siku hiyo.


KWANINI? Ni kwa sababu wanapewa baraka kwa vipaji waliovileta. Hivyo waamini wengine hawapaswi kabisa kupiga Ishara ya Msalaba.


• Hata wakati wa kupokea Ekaristi Takatifu, kuna baadhi ya waamini hupiga Ishara ya Msalaba kabla ya kuila na hata baada ya kuila wakati wa sala ya Mtakatifu Inyasi. Nayo pia hairuhusiwi.


• Hivyo unashauriwa, baada ya kupokea Ekaristi Takatifu, kwa heshima mbele ya Yesu, unapaswa kuinama na kisha kwenda kwenye seat yako na kupiga magoti kwa ajili ya kumshukuru Mungu. Sala inayopaswa kusaliwa muda huo ni ya Mtakatifu Inyasi, ila sala zako binafsi inaruhusiwa, katika hilo hakuna kizuizi.


• Mwisho napenda kusema, wakati wa Misa kuna waamini wengi, hupenda kusali Sala ya Baba yetu huku mikono yao yakiwa yamefunguliwa juu kama Padre. Na hiyo pia haitakiwi, bali mikono yako yako ifumbwe kwa pamoja na sio kuifumbua mikono yote miwili kama Padre anavyofanya. Kwa sababu mwenye mamlaka ya kufanya hayo ni Padre na sio wewe.


• Vilevile hata wakati wa Amani, sio wakati wa kuzungumza na jirani yako kuhusu habari za nyumbani. Bali ni wakati kupeana upendo wa Kimungu kwetu kama Yesu alivyotuagiza. Kupiga makelele wakati wa Amani, unamtoa mtu katika uwepo wa Mungu.


• Hivyo nahitimisha kwa kusema: Ishara ya Msalaba wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ni mbili tu, nazo ni:-

(a) Mwanzo wa Misa.

(b) Mwisho wa Misa.


• Lakini kama kuna maji ya baraka mlangoni unaruhusiwa kupiga Ishara ya Msalaba, na kama hakuna, basi hauruhusiwi tena kupiga Ishara ya Msalaba zaidi ya mara mbili (mwanzo na mwisho wa Misa)


√√√ Ndugu zangu nimeamua kuandika haya, ni kwa sababu waamini wengi hatujui maana wala umuhimu wa Msalaba. Tena mbaya zaidi wakati wa Misa ikiendelea, wengi wetu huwa tunapenda kupiga Ishara ya Msalaba mara nyingi, tukidhani tuko sahihi kumbe tunakosea.


√√√ Natumaini baada ya kuyasoma haya utabadilika, ila usisahau #kushare ujumbe huu ili wengine nao wapate kujua.


√√√ UKINIKANA MBELE ZA WATU, NAMI NITAKUKANA SIKU YA MWISHO MBELE YA BABA YANGU ALIYE MBINGUNI.


√√√ Hivyo, usiogope kupiga Ishara ya Msalaba kokote pale uliko, hata kama umezungukwa na watu wengi wa aina gani.


...Nawatakia Kwaresma Njema...

Joseph

Karibu tuweze kujadili na kupakua habari mpya zilizojili Afrika, Tanzania na pia hata Kidunia kwa ujumla

Chapisha Maoni

I, (taja jina lako/indicate your name)

Mpya zaidi Nzee zaidi