Na Joseph E. Lugembe
Louis Miquissone |
KAMA kweli Simba ikipata mkwanja inaotaka kwa staa wao, Luis Jose Miquissone huenda ikaandika rekodi ya dau ambalo halijawahi kutokea kwenye usajili katika siku za hivi karibuni.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba kimethibitisha kwamba kiwango ambacho alionyesha Miquissone katika mechi ya Al Ahly kimewaibua matajiri wengi Afrika ambao wanamiliki timu mbalimbali na kutaka huduma ya mchezaji huyo.
Miongoni mwa timu ambazo zimeshaonyesha nia ya wazi wazi kwa Simba na kuulizia mkataba wa Miquissone ukoje ni Al Ahly, CD Belouizdad ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Sauzi.
“Ukiachana na timu hizo tatu ambazo zimeonyesha nia ya kumtaka mchezaji wetu na kuulizia upatikanaji wake pamoja na mkataba wake ulivyo kuna nyingine kutoka Misri, Morrocco, Algeria na Afrika Kusini,” alidokeza mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba.
“Lakini nataka nikwambie sisi kwenye vikao vya ndani tumekubaliana kwamba dau la chini kabisa kumuuza huyo mchezaji ni Dola 1 milioni (Sh2.3Bilioni)hicho ndio kigezo cha kwanza,” alisema.